Saturday, June 15, 2013

YAKO WAPI MAPENZI

Yako wapi mapenzi, uliyonipa tangiepo,
ukanitia uchizi, moy'angu ukauteka,
maisha yakawa matamu, honey likawa jina,
rudisha wako moyo, tuishi kama zamani.

vionjo ulivyonipa, adhimu kwa wengine
nkasahau katukatu, karaha za mapenzi
ukazidi nichanganya, kwa mungu nikaapa
Rudisha wako moyo, tuishi kama zamani

kwa mikogo n'katembea, mbele ya wenzangu
jeuri nikajijengea, ninaye mke mwema
hakika sikuiota, siku n'takayotendwa
Rudisha wako moyo, tuishi kama zamani

wenzangu zikawapaa, mioyo mpwitompwito
likawatia wazimu, wakazidi chachalika
chokochoko wakatia, penzile' kuharibu
Rudisha wako moyo, tuishi kama zamani

kwangu ukajiapiza, hutong'atuka katu!
nanga kwangu umetia, mithili manowali
wazimu nikajitia, manenoyo n'kasadiki
Rudisha wako moyo, tuishi kama zamani

hakika sikujua, maneno ya wahenga,
kila king'aacho, 'sidhani ni dhahabu
kivumacho hakidumu, msumari wakapigia
Rudisha wako moyo, tuishi kama zamani

maneno ya wapambe, yakaanza kukulevya
ukaanza kukacha, penzi njiani kutelekeza
ukaniacha ka' hayawani, kinda la dege tawini
Rudisha wako moyo, tuishi kama zamani

roho i radhi, bali mwili dhaifu
penzilo siwezi hacha, pekee n'kaishi
utanitia wazimu, kitanzi nijitie
Rudisha moyo Pepe, tuishi ka'zamani

Nani alokuloga, Pepe ukasaliti
moyoni nitoa, ukasahau zamani
ukajitia ukiziwi, kutosikia hiki kilio
Haya hii pen, nakuandikia mpenzi

Hakika nimekua, ya wakubwa 'meng'amua
mla mla leo, mla jana kala nini?
japo jana nilikula, mwenzio leo ni' taabuni
Rudisha wako moyo tuishi kama zamani

Mwandishi/mtunzi: John Jonas R.

Thursday, June 6, 2013

PEPE BINTI MAYUNGA

U binti uliyeumbika, mfano hakunaga
Mtoto unachanua, mfano wa maua
Yako sura tamu, mfano wa asari
Njoo kwangu malkia, uponye wangu mtima.

Sio siri umeniteka, sina budi kukiri
Haraka moyo waupeleka, kwako sijihimu
Unapendeza unapendeka, nakiri hili bayana

Sifa zo zaimbwa, kote zimeenea
Jinsi ulivyoumbika, mfano hakunaga
Macho yako hata mdomo, hata kipofu avutiwa
Njoo kwangu malkia, uuponye wangu mtima.

Si mfupi mrefu, waswahili eti wastani
Si mnene si mwembamba, bao umewafunga
Uzuri wako wasambaa, kama moto nyikani
Kila mtu ajihisi bahati, kuzungumza na wewe

Nimezunguka bara, nikaenda kule zanzibar
Kote mezunguka, mikoa ishirini na saba
Bado namba moja, chati washikilia
Wanukia wavutia, kama nguva baharini

Kifua mbele tembea uzuri jivunia
Muumba kakutunuku kakidhi yako haja
Wavutia mfano twiga, mbugani manyara

Lakini kumbuka, majivuno ondoa
Kiburi si maungwana, wengine susia
Jifanye nao sawa, japo sio sawa
Njoo kwangu malkia, uuponye wangu mtima.

Pepe wewe Pendo, mtoto umebalikiwa
Umbo lako safi, kama malaika nasema
Umewatoa nishai, wengi macho juujuu
Njoo kwangu malkia, uuponye wangu mtima

Rangi yako kama dhahabu, unawaka kama lulu
Ngozi yako raini, kama mwana paa sikia
Mguu chupa ya bia, hakuna mpinzani najua
Njoo kwangu malkia, uuponye wangu mtima.

Mwenzio niko taabuni, kwa pendo lako tamu
Kila leo ni mpya, mautundu kukazia
Wanipa kila kitu, mfano wa mwana kwa mamaye
Kila nikuonapo mimi hoi, moyo waupeleka mchaka

Mimi nimeanza, wengine watakiri
Hata wasiokiri, wivu wawashika
Wewe ni namba moja, zaidi yako hakuna
U mkari, mzuri wavutia, kama wewe duniani hakuna

Mwisho namaliza, hili zingatia
Sura hapana tisha, tabia myenendo pia
Shika maadiri bora, vigezo vyote timiza
UISHI KWA PENDO DUNIA YA MOLA