Sunday, May 27, 2012
MAVAZI NA UTAMADUNI WA MWAFRIKA
Nimerejea tena uwanjani. Ni katika kudadisi na kudadavua hili na lile. Leo ninalo suala moja tu nalo ni hili, "Lipi vazi linatufaa kama vazi la taifa".
Ninaposikia yakuwa kuna mpango wa watanzania kuletewa vazi la taifa ninapata shaka kiduchu! Hivi watanzania wa leo ususan vijana wanaotamani kutembea uchi wa mnyama barabarani watakubali kuvaa vazi hilo la taifa?
Kila nikijaribu kuwaza sana majibubu yanazidi kuwa mbali zaidi. Hivi utamaduni wa mwafrika tumeutupa wapi? Suala gani limezifanya mila zetu za zamani kufukiwa shimoni na kuiga yale ya wageni! Sisi mbona tunatia huruma jamani. Tunaukataa usisi na kuutukuza uwale! Huu ni upuuzi usiokuwa na msingi wowote.
Dada zetu nani amewaloga. Au msemo nyinyi ni maua nanyi mmesadiki. Kitu gani kinawafanya mtembee barabarani mkiwa uchi? Mbona mmesahau haya, au hamjui yakuwa nyinyi ni wazuri. Yaani mnapendeza hata msipojiremba. Sasa nyinyi badala ya kujilemba mnatembea uchi! Lo!
Mimi niseme hakuna mwanadamu aliyeumbwa na maungo ya kuvutia kama mwafrika (binti). Sasa kitu gani kiwafanye mjiuze miili yenu sokoni kama dagaa wa Kigoma wakati nyinyi ni lulu? Na hayo maziwa yenu mbona mnayafunga Tanganyika jeki nyinyi mnasema eti mna boost kidogo! Huu ni upuuzi kabisa. Wengine mnatumia dawa kuongeza ujazo wa maziwa yenu! Mmelogwa?
Yaani maziwa yakituna tena yakawa nje ndo mnapendeza? Hapo mmedanganywa mkadanganyika. Tena mnazo nguo mnaziita bluetooth. Yaani hizo mkivaa tunaona ama chup au tight. Iz it fair? Binti kupanda daladala watu uwape shida, ya nini?
Sasa kuna mtindo mpya. Eti mnasema taiti ndefu. Mwana dada kakupigia hiyo taiti ndefu na ki-topu. Ehh! Barabarani utadhani mwenda wazimu anapita!
Nanyinyi kaka zangu huu mtindo mmejifunza wapi? Hii nyinyi mnaiita kata kei. Sasa ndo kusema suruali haziwatoshi tena au ndo kutaka kurahisisha mambo? Mwanamume unamvutia nani na wewe? Umevaa nguo ya nje lakini chupi, boxer viko nje! Yaani kijana akiinama aibu. Sasa kama binti anafanya hivyo kutafuta soko wewe mwanamume unatafuta nini? Mimi nnavyo jua dume ndilo malanyingi linatongoza baada ya kuvutiwa! Sasa wewe na harakati za kutembea uchi mwanamume ni nini?
Ndugu zanguni tubadilike. Tusiyatupe maadili kwa kuiga mambo ya kigeni. Sawa hata mkitaka kujifunza baadhi angalia ni nini! Mbona hata mazuzu huchagua waokote nini jaani na sio kila kitu? Tubadilike; mabadiliko yanaanza na wewe. Fanya hivyo.
Jonas John R.
ISW
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment