KATIKA ZOEZI ZIMA LA VITAMBULISHO VYA UTAIFA, NIDA MMEKURUPUKA.
Ni hivi karibuni ambapo taifa letu limeingia katika mchakato wa kutoa vitambulisho vya utaifa kwa wakazi wote nchini na watanzania wote.
Zoezi hili linasimamiwa na taifa chini ya wakala wa vitambulisho vya taifa NIDA. Kusema kweli NIDA wamekurupuka katika kuanzisha utekelezaji wa mpango huu wakianza na mkoa wa Dar es salaam. Pamoja na yakuwa siku walizotoa hapo hawali kutotosha bado NIDA hawakufanya tathmini ya hawali kujua idadi ya wakazi katika vitongoji vya mkoa huu.
Zipo sehemu zenye wakazi wengi kupindukia na bado wameweka kituo kimoja cha kuandikia watu katika kata moja. Hili limezua fujo katika vituo hivyo watu wakigombea kuandikwa. Wakazi wa jiji la Dar es salaamu kwa siku kadhaa sasa wameailisha shughuli zao za msingi wakishinda katika mistari wakingoja kuandikwa.
Aidha, mbali na kuwa vituo vya uandikishaji kufunguliwa asubuhi ya saa mbili, watu wamekuwa wakifurika vituoni hapo tangu saa kumi usiku kuwai kile wanachokiita namba.
Pamoja na adha hii, bado kumekuwa na utaratibu mbovu unaoshindwa kuwabaini watu waliowai. Hali hii imesababisha watu kutumia nguvu zaidi katika zoezi hili badala ya utaratibu na utu.
Zoezi hili limeonekana pia kuvutia rushwa kwa watendaji na kutoa huduma kulingana na mtu anavyojulikana.
Ni ombi langu sasa NIDA watakapokuwa wameamishia zoezi hili mikoani wajitaidi kuboresha huduma zao ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi vituoni kulinda usalama wa raia. Pia NIDA wajaribu kufikiria uwezekano wa kuandikishwa na kupiga picha kwa wakati mmoja. Mbali na kwamba zoezi hilo litaokoa muda bado gharama za uendeshaji na usumbufu vitapungua.
Niseme, vitambulisho vya utaifa ni suala la maana sana. Ni vyema kila raia kujiandikisha kupata utambulisho huu. Utaratibu ubooreshwe ili kutoa mwanya kwa watu wengi kujiandikisha. Vituo vya kujiandikisha viwekwe vingi kulingana na uwingi wa watu wa eneo.
No comments:
Post a Comment